Thursday, November 19, 2015

Kijana Afariki Dunia Baada ya Kufanya Mapenzi na Nguruwe Wilayani Ludewa

Kijana mmoja aitwaye Simon Dustan Mwanjavala maarufu kama Mwachakala (15) mkazi wa kijiji cha Mbwila kata ya Luana wilaya ya Ludewa mkoani Njombe amefariki dunia muda mchache baada ya kukutwa akifanya mapenzi na Nguruwe

Tukio hilo la kustaajabisha limetokea leo wilayani Ludewa baada ya kijana huyo "kufumaniwa" akifanya mapenzi na mnyama huyo, ndipo walipomkamata na kumfunga kamba mikono yake na miguu ili asikimbie.

Baada ya majirani kumuona kijana huyo akimbaka nguruwe huyo kwenye banda la mnyama huyo walikwenda kumwambia baba yake mdogo ambao kwa pamoja walimkamata kijana huyo, ambaye alikiri kufanya kosa hilo
Alipoulizwa sababu zilizomfanya kufanya mapenzi na nguruwe, alisema alikuwa na hamu ya kufanya tendo hilo.

Kutokana na kitendo hicho waliamua kumvua nguo zote na kumfunga kamba na kumpa kichapo  kisha wakamuacha kwa muda kwenye eneo la tukio, na walipokuja kumfungua kamba na mwenyekiti wa kijiji hicho, alidondoka na kufariki dunia papo hapo
Mpekuzi blog

Rais Magufuli Amteua Kassim Majaliwa Kuwa Waziri Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amemteua mbunge wa jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa kuwa waziri mkuu wa serikali ya awamu ya tano.

Uteuzi huo umetangazwa Bungeni alhamisi hii na spika wa bunge, Job Ndugai aliyesoma barua iliyoandikwa kwa mkono na Rais  Magufuli.

Kabla ya hapo, mh Majaliwa alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri MkuuTawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI).

Bunge limesimama kwa muda kupisha mchakato wa wabunge kuthibitisha uteuzi huo.

Mheshimiwa Majaliwa alizaliwa December 22, 1960.

Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Waanza Kuhojiwa na Polisi Kwa Kuvuruga Uchaguzi

Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), wameanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kuvurugika kwa Uchaguzi Mkuu na kusababisha Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka huu.

Viongozi waliohojiwa na Polisi  ni Makamishna na Watendaji wa tume hiyo akiwamo Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Issa Ameir.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alithibitisha mjini hapa Mjini jana kuwa Makamishina wa Zec na Watendaji, wameanza kuhojiwa na maofisa wa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema hadi sasa uchunguzi umefikia hatua kubwa na baada ya kukamilika, majalada ya uchunguzi yatapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, kabla ya wahusika kufikishwa mahakamani.

“Tunawahoji Makamishna na Watendaji wa Tume, Makamu Mwenyekiti yeye tayari tumemhoji, bado Mwenyekiti na maofisa wengine,” alifafanua DDCI Msangi.

Alisema Polisi waliingia kazini baada ya kuripotiwa kuwa uchaguzi umevurugwa na kazi inayofanyika ni kukusanya ushahidi na vielelezo kabla ya wahusika kufunguliwa mashitaka kwa kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Alisema uchunguzi huo umegawanyika sehemu tatu na kuwahusisha Tume, waathirika na wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha, alisema kuna mambo mazito yameanza kuonekana tangu kuanza kufanyika kwa uchunguzi, lakini alisema ni mapema kueleza uchunguzi huo utachukukua muda gani kukamilika.

"Wahusika watafikishwa mahakamni baada ya majalada ya uchunguzi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar kabla ya kufikishwa mahakamani," alisema Msangi.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi huyo alisema hali ya Zanzibar ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida tangu Zec ilipofuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Akitangaza kufuta uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Zec, Jecha alisema kuna sababu tisa zimemfanya kuchukua hatua hiyo.
Alizitaja kuwa ni pamoja na vituo vya wapigakura na idadi ya kura katika visanduku zilikuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliosajiliwa katika daftari la wapigakura katika vituo vya uchaguzi.

Aidha, alisema kuna visanduku vya kura viliporwa na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na sheria pamoja na mawakala wa vyama kupigwa na kufukuzwa katika vituo vyao vya kazi siku ya uchaguzi.

Tayari Zec imetangaza rasmi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu kufutwa kwa uchaguzi huo na kuwataka wananchi kusubiri kutangazwa tarehe ya kurudiwa.

Dr.Tulia:Sijapandikizwa ili Niibebe Serikali

Mgombea unaibu spika kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Tulia Ackson Mwansasu, amekanusha madai kwamba amepewa nafasi hiyo kama pandikizi ili aibebe Serikali.

Amesema madai kuwa ataibeba Serikali kwa kuwa ni mbunge wa kuteuliwa hayana msingi kwa kuwa haendi bungeni kumtumikia rais bali kuwatumikia Watanzania.

Rais John Magufuli Jumatatu wiki hii alimteua Dk. Ackson kuwa mbunge wa kuteuliwa na kutengua nafasi yake ya naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali aliyoteuliwa hivi karibuni na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

“Ni kweli nimeteuliwa na rais, lakini nakwenda kufanya kazi za Watanzania, nikipata nafasi ya kuwa naibu Spika madai kuwa nitaibeba serikali hayapo kwa kuwa nitafanya kazi za Bunge ambazo ni kuisimamia, kuishauri na kuiwajibisha serikali,” alisema Dk. Ackson ambaye juzi usiku alipitishwa kwa kauli moja na wabunge wa CCM kuwa mgombea wake wa unaibu spika.

Alisema ni vyema wabunge wakawa na imani naye na kumpa ushirikiano wa dhati ili atekeleze majukumu yake ipasavyo.
Katika hatua nyingine, vita ya unaibu Spika wa Bunge la 11, imemalizika, baada ya, Dk. Ackson, kupitishwa kwa kauli moja na wabunge wa CCM kugombea nafasi hiyo.

Awali kulikuwa na mvutano wa ndani kwa ndani baina ya wabunge wa chama hicho, ambao waligawanyika kwa baadhi kumtaka Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.

Bomoabomoa yaacha vilio na simanzi Dar


Manispaa ya Kinondoni jana ilisababisha vilio kwa wakazi wa maeneo wa wilaya hiyo ilipoanza ubomoaji wa nyumba zilizojengwa maeneo ya wazi na hifadhi kinyume cha sheria

Juzi, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusirika alitangaza operesheni ya kubomoa nyumba hizo kuanzia jana na kuwa baada ya Kinondoni watahamia wilaya nyingine na mikoani pia.

Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na bomoabomoa hiyo jana ni Mwenge, Sinza, Biafra-Bwawani na Mivumoni.

Huku baadhi wakiangua vilio, wakazi waliokumbwa na hatua hiyo walilalamika wakidai hawakuwa na taarifa za kuwapo kwa ubomoaji huo, jambo lililosababisha baadhi yao kushindwa kuokoa mali zilizokuwa ndani.

Tuesday, November 17, 2015

Mtu Mwingine Auawa Kinyama Geita... kifo chake Utata Mtupu

Mtu ambaye hajafahamika jina wala makazi, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Katoro wilayani Geita, baada ya kufikishwa na polisi akiwa hajitambui.

Mtu huyo anasadikika kupigwa na watu wasiojulikana Jumamosi saa mbili usiku, huku tukio hilo likihusishwa na chuki za kisiasa zinazohusiana na vurugu zilizosababisha kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Daniel Izengo alisema 
saa 2:30 usiku walimpokea mtu huyo aliyefikishwa na polisi akiwa na majeraha makubwa sehemu za kichwani.

Awali, mganga huyo alisema watu wawili walijeruhiwa katika vurugu zilizosababisha kifo cha Mawazo ambao walifikishwa kwenye kituo hicho wakatibiwa na kuruhusiwa.

Pia alisema watu watatu walifikishwa kituoni hapo juzi akiwamo Mawazo, Elizabeth Paschal (48) na Bahati Michael (38) wote wakiwa wakazi wa Katoro.

Dk Izengo alisema hali ya Mawazo ilibadilika na 
kumwandikia rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Geita ambako alifariki dunia, huku majeruhi wengine wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa baada ya hali zao kuridhisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lotson Mponjoli alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea, ikiwamo kuwatafuta watuhumiwa.

Hilo ni tukio la pili ndani ya siku chache, la kwanza likiwa la kifo cha Mawazo.

Sakata la Mkuu wa Majeshi Kulishwa Sumu: Serikali Yakata Rufaa Kupinga Mshitakiwa Kupewa Dhamana

Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Tanzania (DIT), Benedict Ngonyani, anayetuhumiwa kusambaza taarifa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali, Davis Mwamunyange, amelishwa sumu, umewasilisha mahakamani kusudio la kukata rufaa kupinga mshtakiwa huyo kupewa dhamana.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, ilitengua hati ya kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP). 
 

Kabla ya uamuzi huo, hakimu alisikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili na alikubaliana na maombi ya utetezi ya kumpa dhamana kwa kuwa sababu za DPP kuzuia dhamana hiyo hazikuwa na msingi wa kisheria. 

Wakili wa Serikali Mkuu, Theophil Mutakyawa aliwasilisha kusudio hilo jana saa 7:00 mchana, kwamba upande wa Jamhuri haujaridhika na uamuzi wa mahakama kutengua hati ya DPP. 
 

Pia, kupitia kusudio hilo, upande wa Jamhuri unapinga Mahakama ya Kisutu kutengua hati hiyo na kwamba haina mamlaka ya kuoindoa kwa kuwa huondolewa na DPP ama kesi inapomalizika na kutolewa hukumu.

Awali hakimu alisema mshtakiwa ni mwanafunzi na shtaka analoshtakiwa nalo linadhaminika kwa hiyo haoni haja ya kukosa masomo yake ya darasani

Katika kesi hiyo, inadaiwa Septemba 25, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alisambaza taarifa za uongo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu cha 16 ya mwaka 2015 kuwa Jenerali Mwamunyange amenyweshwa sumu.

Serikali Kuwabeba Wanafunzi Wanaofeli Form Two na Darasa la Nne

Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakianza mitihani jana, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza kwamba wanafunzi watakaofeli mtihani huo hawatorudia darasa, bali wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya jioni ili kuwawezesha kitaaluma.

Utaratibu huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha wastani wa alama 30.

Dk Msonde alisema utaratibu huo mpya utawahusu pia wanafunzi wa darasa la nne ambao nao hawatalazimika kurudia darasa, bali watakuwa na muda wao wa ziada wa kusoma.

“Lengo la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya ufundishaji. Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na siyo kuwarudisha darasa tu,” alisema.

Akizungumzia mtihani huo ulioanza jana, alisema watahiniwa 397,250 walisajiliwa nchi nzima, wakiwamo wanafunzi 67 wasioona na 224 wenye uoni hafifu.

Mwaka 2008, Serikali ilifuta makali ya mtihani wa kidato cha pili, hali iliyotoa fursa kwa wanafunzi wengi hata wasio na uwezo kuingia kidato cha tatu na hatimaye kupata nafasi ya kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.

Baada ya matokeo mabaya yaliyotokana na uamuzi huo na pia kelele za wadau wa elimu na jamii kwa jumla, hatimaye mwaka 2012, Serikali iliurudisha mtihani huo na kutangaza kuwa wanaofeli watakariri darasa, utaratibu ambao sasa umefutwa.
Mpekuzi blog

Job Ndugai: Tutegemee Migomo Katika Bunge Hili la 11


Baada ya kuteuliwa na CCM na kupita katika mchakato wa kumpata mgombea Uspika wa Bunge la Kumi na moja bila kupingwa, Job Ndugai ameeleza changamoto anazotarajia kukutana nazo ikiwa ni pamoja na migomo.

Akiongea na waandishi wa habari jana baada ya jina lake kupitishwa, Ndugai alilielezea Bunge la kumi na moja kama Bunge lenye utofauti mkubwa na mabunge mengine huku akidai kuwa ongozeko la vijana wengi na wasomi wengi zaidi kunaashiria kuongezeka kwa changamoto zaidi.

“Bunge hili lina wabunge wengi vijana, lina wabunge wengi wasomi zaidi kuliko mabunge yote yaliyowahi kutokea na lina uwakilishi mkubwa. Hili ni Bunge ambalo litakuwa na changamoto nyingi, tetegemee migomo ya hapa na pale, hata hivyo ubora wa kazi utakuwa mkubwa,” alisema Ndugai.Hata hivyo, Ndugai alisisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa weledi na kutenda haki kwa kila upande hivyo aliwataka wabunge wote wakiwemo wa upinzani kumuunga mkono leo ili awe Spika wa Bunge la 11.

Monday, November 16, 2015

CCM Yapitisha Majina Matatu ya Wagombea Uspika......Samwel Siita, Emmanuel Nchimbi Out!!!


Kamati Kuu CCM imewapitisha Job Ndugai, Abdullah Ali Mwinyi na Dr. Tulia Ackson Mwansasu kugombea nafasi ya Uspika wa Bunge la 11.
 
Majina hayo yamepenya kutoka katika orodha ya majina 21, miongoni mwao akiwemo Spika wa Bunge la 9, Samuel Sitta, Dkt. Didas Masaburi ambaye alitangaza kujitoa katika dakika za mwisho, Dkt Kalokola na wengineo.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jioni ya leo baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichoongozwa na mwenyekiti wake Dkt Jakaya Kikwete mjini Dodoma, jina moja kati ya hayo matatu litatangazwa kesho Jumatatu ikiwa ni pamoja na jina la mgombea wa nafasi ya Naibu Spika.
 
Katika waliopitishwa:
Job Ndugai ni mbunge mteule jimbo la Kongwa Dodoma na pia alikuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita.
 
Dkt Tulia Ackson ni Naibu Mwanasheria mkuu wa serikali, pia alikuwa ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba akitokea taasisi za elimu ya juu. Amekuwa mhadhiri wa sheria katika kitivo (sasa shule) cha sheria chuo kikuu cha Dar es salaam.
 
Abdullah Mwinyi ni mtoto wa Rais mstaafu Al Hajj Aly Hassan Mwinyi na ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

KOVA: Mita 200 za UKAWA Zilitunyima Usingizi


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna, Suleiman Kova amesema kati ya masuala ambayo yaliliumiza kichwa Jeshi la Polisi ni maagizo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa wafuasi wao.

Kova alisema suala ambalo liliwanyima zaidi usingizi ni maagizo ya maandamano baada ya uchaguzi pamoja na wananchi kutakiwa kulinda kura zao mita 200, kutoka katika vituo vya kupigia kura.
  
 “Lakini tunashukuru kwa kumaliza Uchaguzi Mkuu salama na hakuna aliyeyapokea maagizo hayo,” alisema.

Akizungumza katika hafla maalumu ya kuwapongeza askari wake kwa kusimamia vema kampeni na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, Kova alisema maagizo ya kulinda kura mita 200 na suala la maandamano bila kikomo yaliumiza vichwa jeshi hilo.

Kova alisisitiza kwamba japokuwa usimamizi wa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa mgumu na wa hatari tofauti na mwingine wowote uliowahi kufanyika nchini tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, walitoa nafasi sawa za ulinzi na uongozaji wa misafara ya wagombea wote bila kutoa upendeleo, hivyo kuonyesha mfano.

Alisema kwa mara ya kwanza uchaguzi umemalizika salama bila kuwapo kwa vifo au majeruhi yaliyosababishwa na polisi, kutokana na askari kutambua wajibu wao kwa wananchi na kutumia muda mwingi kutoa elimu zaidi bila ya kutumia nguvu.

Kova alieleza kuwa japokuwa kulikuwa na mazingira ya kuchokozwa kwa makusudi, polisi waliweza kuvuka kizingiti hicho na kusimamia vema uchaguzi huo.

Alisema hatua inayofuata ni kuhakikisha askari hao wanalipwa stahili hasa posho zao ambazo hawakulipwa wakati wote wa kampeni na kusimamia uchaguzi.

Alisema agizo hilo amelitoa kwa wahusika na kwamba limeanza kufanyiwa kazi. Kamanda Kova alisema sasa wanajielekeza kupambana na uhalifu.

Saturday, November 14, 2015

Pigo CHADEMA: Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita Auawa kwa Kukatwa Mapanga


Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo ameuawa leo mjini Katoro baada ya kushambuliwa kwa mapanga na shoka na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimali za mwili wake hasa kichwani wakati akifanya kampeni za kumnadi diwani wake

Mawazo aliyewahi pia kuwa Diwani wa Kata ya Sombetini Arusha amefariki dunia akiwa hospitalini alipokimbizwa katika jitihada za kujaribu kuokoa maisha yake. Mganga Mkuu Geita amethibitisha.